Genesis 13

Abramu Na Lutu Watengana

1 aHivyo Abramu akakwea kutoka Misri kwenda Negebu, yeye na mkewe na kila kitu alichokuwa nacho, pia Lutu akaenda pamoja naye. 2 bWakati huo Abramu alikuwa tajiri sana wa mifugo, fedha na dhahabu.

3 cKutoka Negebu, akapita mahali hadi mahali, hadi akafika Betheli, mahali hapo ambapo mwanzoni alipiga hema lake kati ya Betheli na Ai 4 dhapo ambapo alikuwa amejenga madhabahu ya kwanza. Huko Abramu akaliitia jina la Bwana.

5 eBasi Lutu, ambaye alikuwa anafuatana na Abramu, alikuwa pia na makundi ya mbuzi, kondoo, ng’ombe na mahema. 6 fLakini nchi haikuwatosha kukaa pamoja kwa ajili ya wingi wa mali zao. 7 gUkazuka ugomvi kati ya wachunga mifugo wa Abramu na wale wa Lutu. Wakati huo, Wakanaani na Waperizi ndio waliokuwa wenyeji wa nchi hiyo.

8 hHivyo Abramu akamwambia Lutu, “Pasiwe na ugomvi wowote kati yangu na wewe, wala kati ya wachungaji wangu na wako, kwa kuwa sisi ni ndugu. 9 iJe, nchi yote haiko mbele yako? Tutengane. Kama ukielekea kushoto, nitakwenda kulia; kama ukielekea kulia, mimi nitakwenda kushoto.”

10 jLutu akatazama akaona lile bonde lote la Yordani kuwa lilikuwa na maji tele, kama bustani ya Bwana, kama nchi ya Misri, kuelekea Soari. (Hii ilikuwa kabla Bwana hajaharibu Sodoma na Gomora.) 11Hivyo Lutu akajichagulia bonde lote la Yordani, akaelekea upande wa mashariki. Watu hao wawili wakatengana: 12 kAbramu akaishi katika nchi ya Kanaani, wakati Lutu aliishi miongoni mwa miji ya lile bonde na kupiga mahema yake karibu na Sodoma. 13 lBasi watu wa Sodoma walikuwa waovu, wakifanya sana dhambi dhidi ya Bwana.

14 mBaada ya Lutu kuondoka Bwana akamwambia Abramu, “Ukiwa hapo ulipo, inua macho yako utazame kaskazini na kusini, mashariki na magharibi. 15 nNchi yote unayoiona nitakupa wewe na uzao wako hata milele. 16 oNitaufanya uzao wako uwe mwingi kama mavumbi ya nchi, hivyo kama kuna yeyote awezaye kuhesabu mavumbi, basi uzao wako utahesabika. 17 pOndoka, tembea katika marefu na mapana ya nchi, kwa maana ninakupa wewe.”

18 qBasi Abramu akaondoa mahema yake, akaenda kuishi karibu na mialoni ya Mamre huko Hebroni, huko akamjengea Bwana madhabahu.
Copyright information for SwhKC